Ng'ombe (kundinyota)

(Elekezwa kutoka Tauri (kundinyota))

Ng'ombe (pia Tauri, kwa Kilatini na Kiingereza Taurus) [1] ni jina la kundinyota kwenye nusutufe ya kaskazini ya dunia yetu.

Nyota za kundinyota Ng'ombe (Tauri - Taurus) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Tauri - Taurus jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini
Ng'ombe - Tauri jinsi ilivyowazwa na mwanaastronomia Al-Sufi

Mahali pake

Ng'ombe iko angani kwenye mstari wa Zodiaki kati ya Kondoo (pia Hamali, lat. Aries) upande wa magharibi na Mapacha (pia Jauza, lat. Gemini) upande wa mashariki.

Inapaka na kundinyota jirani za Hudhi (Auriga), Farisi (Perseus), Hamali (Kondoo) (Aries), Ketusi (Cetus), Nahari (Eridanus), Jabari (Orion) na Jauza (Mapacha) (Gemini).

Ng'ombe - Taurus ni sehemu ya zodiaki maana yake mstari wa ekliptiki unapita humo. Ilhali miendo ya Mwezi na sayari inafuatana karibu na ekliptiki magimba haya huonekana katika eneo la Tauri kwa wakati fulani kwenye mwaka.

Jina

Ng'ombe ni tafsiri ya Tauri. Mabaharia Waswahili walijua nyota hili tangu miaka mingi kwa jina Tauri. Walipokea jina hili kutoka Waarabu wanaosema ثور thawr ambalo linamaanisha fahali[2]. Waarabu walitafsiri hapa jina la Ptolemaio aliyetaja nyota hizi vile kwa jina la Ταῦρος tauros yaani fahali katika orodha yake ya Almagesti[3].

Wagiriki wa Kale waliwahi kupokea kundinyota hili likiangaliwa kama fahali kutoka utamaduni wa Babeli. Katika mitholojia ya Wagiriki kuna hadithi mbalimbali zilizosimuliwa hapa. Hasahasa waliona fahali kwenye anga kama ishara ya mungu mkuu Zeus aliyechukua umbo la fahali alipomtongoza binti Europa; Zeus alibadilisha umbo lake akaingia katika kundi la ng'ombe waliochungwa na Europa. Siku mmoja Europa alipanda juu ya fahali na hapo Zeus alikimbia naye hadi kisiwa cha Kreta; hapa alizaa naye wana watatu akamfanya Europa malkia wa kwanza wa Kreta. Aliweka umbo la fahali kati ya nyota kama kumbukumbu ya mapenzi yake.

Katika unajimu wa kisasa katika Afrika ya Mashariki jina "Tauri" limesahauliwa badala yake kundinyota hili linaitwa kwa tafsiri tu ya "Ng'ombe".

Ng'ombe - Taurus ni kati ya makundinyota 48 zilizotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika kitabu cha Almagesti wakati wa karne ya 2 BK. Iko pia kati ya makundinyota 88 yanayoorodheshwa na Umoja wa kimataifa wa astronomia [4] kwa jina la Taurus. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Taui'.[5]

Nyota

Nyota za Ng'ombe huwa haziko pamoja kihalisi lakini zinaonekana tu vile kutoka duniani. Kwa uhalisi kuna umbali mkubwa kati yao, kama ziko mbali au jirani nasi. Kwa hiyo kundinyota "Ng'ombe" linaonyesha eneo la angani jinsi tunavyoliona kutoka Duniani.

Kuna nyota nyingi katika eneo la kundinyota hili na hasa Dabarani (en:Aldebaran), inaitwa pia Alfa Tauri, ambayo ni nyota jitu jekundu ikiwa kati ya nyota angavu zaidi zinazoonekana angani[6].

Kuna nebula la Messier 1 inayojulikana pia kwa jina la Nebula ya Kaa (en:crab nebula)[7]. Ni mabaki ya nyota nova ambayo mlipuko wake ulirekodiwa huko China mwaka 1054 baadaye pia Japani[8].

Fungunyota la Kilimia (en:Pleiades) linaonekana vema kwa macho matupu katika kaskazini ya Ng'ombe.[9], [10]

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Aina ya spektra
α87Dabarani - en:Aldebaran0,8765K5 III
β112Elnath1,65131B7 III
ηAlcyone2,85368B7 III
ζ123Tianguan3,0ca. 400B2 IVe
θ23,40149A7 III
λ3,41480B3 V + A
εAin3,53155K0 III
ο3,61212G8 III
27Atlas3,62381B8 III
γHyadum I3,65162G8 III
17Electra3,72371B6 III
ξ3,73222B9 Vn
δ1Hyadum II3,77154G8 III
θ13,84158G7 III
20Maia3,87360B8 III
ν3,91129A1 V
Habari za mwangaza na umbali vinaweza kubadilika kutokana na vipimo vipya

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Taurus" katika lugha ya Kilatini ni "Tauri" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Tauri, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. PAL - Glossary "Taurus", tovuti ya mradi wa "Ptolemaeus Arabus et Latinus (PAL)" wa Bavarian Academy of Sciences and Humanities, iliangaliwa Oktoba 2017
  4. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  5. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  6. ALDEBARAN (Alpha Tauri), tovuti ya Prof. Jim Kaler
  7. Nebula ya Kaa haina uhusiano na kundinyota la Saratani linaloitwa pia Kaa. Jina lake lilibuniwa kwa sababu umbo lake lilifanana na kaa.
  8. Why and how did a Japanese poet record the Supernova of AD 1054? Tovuti ya archive.org, iliangaliwa Julai 2017
  9. Taurus], tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Oktoba 2017
  10. Pleiades, tovuti ya Prof J Kaler

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 215 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review

September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331


Makundinyota ya Zodiaki
Majina ya kisasa yanafuatwa kwa mabano na jina la mabaharia na jina la Kilatini (la kimataifa)

Kaa (Saratani – Cancer )Kondoo (Hamali – Aries )Mapacha (Jauza – Gemini )Mashuke (Nadhifa – Virgo )Mbuzi (Jadi – Capricornus )MizaniLibra ) • Mshale (Kausi – Sagittarius )Ndoo (Dalu – Aquarius )Nge (Akarabu – Scorpius )Ng'ombe (Tauri – Taurus )Samaki (Hutu – Pisces )Simba (Asadi – Leo )